Kumbe kupatikana kwa kocha mpya msaidizi wa Simba ilitumika nguvu kubwa mno baada ya kulazimika kupata ushauri kutoka kwa kocha wa nje ya nchi ambaye ndiye aliyepitisha kutua kwa Mganda, Jackson Mayanja kuja kuchukua mikoba hiyo.
Imebainika kuwa Simba ilipokuwa kwenye mchakato wa kutafuta kocha mpya jina la Mayanja liliwazidi wengine waliokuwa kwenye listi hiyo lakini ikalazimika kuulizia tabia za kocha huyo na mwenendo wake kutoka kwa Kocha Mkuu wa Kenya, Bobby Williamson raia wa Scotland.
Mtu wa ndani kutoka sekretarieti ya Simba aliweka wazi kuwa aliyetaka kufanyika kwa zoezi hilo ni kocha aliyefungashiwa virago vyake rasmi jana, Muingereza, Dylan Kerr ambapo hata zoezi la kufanya mawasiliano na Bobby alilifanya mwenyewe.
Imeelezwa kwamba Kerr aliwasiliana na Bobby kwa kutaka kujihakikishia kama Mayanja aliyewahi kuinoa Kagera Sugar na Coastal Union hana majungu na hawezi kuigawa timu. Miaka ya nyuma Mayanja aliwahi kufanya kazi na Bobby akiwa kama kocha msaidizi wa timu ya taifa ya Kenya.
Hata hivyo, Bobby alimhakikishia Kerr kuwa Mayanja ni mtu safi anayeijua misingi ya kazi yake hivyo hana matatizo. Hiyo ikawa ahueni kwa Kerr.
“Kama Mayanja kupitishwa kuifundisha Simba, alishapita tangu siku ile ambayo timu inasafiri kwenda Zanzibar katika Kombe la Mapinduzi lakini ikalazimu kusubiri kwanza kumsikilizia Kerr naye amalize kumuulizia Bobby,” alisema mtoa taarifa huyo.
Hata hivyo, imefafanuliwa zaidi kuwa kama Bobby angediriki kumponda Mayanja basi kungekuwa na ugumu au ungetokea mvutano wa kocha huyo kuanza kazi na Kerr ambaye wakati huo anafanya maamuzi hayo alikuwa hajajua kama atatimuliwa hivi karibuni.
No comments:
Post a Comment