• Seynation Updates

    Sunday, 25 September 2016

    MAJAMBAZI YAKAMATWA MWANZA

    Ahmed Msangi , Kamanda wa Polisi Mkoani wa Mwanza

    MTU mmoja amefariki dunia baada ya kupigwa risasi tatu kifuani, mwingine kujeruhiwa na watu wanaodaiwa kuwa majambazi katika tukio la uharifu wa kutumia silaha za moto mkoani Mwanza, anaandika Moses Mseti.
    Tukio hilo linakuja ikiwa ni miezi miwili tangu kutokea kwa mauaji ya kikatili na ya kinyama mkoani humo, likiwemo la watu watatu kuchinjwa, wakiwa kwenye msikitini wa Rahman.
    Tukio hilo limetokea juzi saa 1:30 hadi saa 1:45 jioni katika Mtaa wa Mecco Kata ya Nyakato jijini humo na kusababisha wafanyabiashara na wakazi wa mtaa huo kufunga biashara zao na kukimbilia kusikojulikana.
    Inaelezwa kuwa, baada ya wahalifu hao wanaokadiriwa kuwa saba kufika katika eneo hilo, walianza kupiga risasi hewani na vilipuzi (fataki) kuwatawanya watu waliokuwa eneo hilo.
    Inaelezwa kuwa, kitendo cha majambazi hao kufika na kuanza kupiga risasi hovyo, kimesababisha Jeshi la Polisi jijini humo kutuhumiwa kushindwa kufika kwa wakati eneo la tukio.
    Wafanyabiashara wawili walioporwa fedha taslimu pamoja na simu, Elizabeth Shayo na Onest Mushi wamesema kuwa, majambazi hao walifikia eneo hilo saa 1: 30 wakiwa kwenye gari dogo jeusi na kuanza kufyatua risasi.
    “Hawa waliofanya uhalifu huu ni vijana wadogo, walifika na kuanza kupiga risasi (huku akionesha sehemu risasi lilipopiga dukani kwake) hapo ndipo watu wakaanza kukimbi na jirani yangu ndipo wakampiga risasi kifuani.
    “Walipompiga jirani yangu risasi na kufanikiwa kuingia dukani na kuchukua pesa zake (kiasi hakijajulikani), walienda kwenye duka la M-Pesa na huko napo walichukua fedha na kutokomea kusikojulikana,” amesema Elizabeth Shayo.
    Amesema kuwa, lawama na tuhuma zote wanazielekeza kwa Jeshi la Polisi kwa kushindwa kufika eneo hilo kwa wakati na kusababisha wahalifu hao kutekeleza azma yao bila hofu.
    Ahmed Msangi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Naibu Kamishna wa Polisi, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kumtaja aliyefariki kuwa ni Grace Maega akiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando (BMC) jijini humo.
    Msangi amesema, “mpaka sasa kiasi cha fedha kilichoporwa na majambazi hao bado hakijafahamika, majambazi walikuwa na bunduki aina ya SMG/ SAR na mwili wa marehemu Maega umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando (BMC),” amesema.
    Kamanda Msangi amesema kuwa, Jeshi la Polisi linaendelea na msako mkali na uchunguzi wa tukio hilo ili kuwabaini watu waliohusika kufanya tukio hilo huku akiwaomba wananchi kutoa ushirikiano kwa polisi.

    No comments:

    Post a Comment

    VIDEO MPYA

    UMBEA MTUPUU

    MAPENZI