UCHAGUZI
wa marudio Zanzibar umefanyika leo, huku Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi
(ZEC), Jecha Salum Jecha, akiwahakikishia Wazanzibari kufanya kila
linalowezekana, ili kuuendesha uchaguzi kwa usalama na amani na
kuhakikisha unakuwa huru na wa haki. Wagombea urais watakaoshiriki
katika uchaguzi huo ni Dk Ali Mohamed Shein wa CCM, Seif Sharif Hamad wa
CUF, Juma Ali Khatib wa TADEA, Khamis Iddi Lilla wa ACT Wazalendo,
Hamad Rashid Mohamed kutoka ADC na Said Soud Said wa AFP.
Wengine
ni Ali Khatib Ali wa CCK, Mohamed Masoud Rashid wa CHAUMMA, Abdalla
Kombo Khamis wa DP, Kassim Bakari Ali wa JAHAZI ASILIA, Tabu Mussa Juma
wa Demokrasia Makini, Seif Ali Iddi wa NRA, Issa Mohamed Zonga wa SAU na
Hafidh Hassan Suleiman wa TLP.
Uchaguzi
huo unafanyika baada ya kufutwa kwa uchaguzi wa Oktoba 25, 2015
kutokana na kasoro zilizojitokeza kama zilivyotangazwa na Jecha, huku
CUF ikitangaza kususa uchaguzi huo. Wakati uchaguzi huo unafutwa, CCM
ilishashinda viti vya uwakilishi kwenye majimbo 27 na CUF pia ilishinda
majimbo 27 na wawakilishi walioshinda walikabidhiwa hati ya ushindi,
lakini kutokana na kasoro ambazo Tume ilibaini uchaguzi huo ukafutwa.
ZEC
yatoa utaratibu Tamko la ZEC kuhusu uchaguzi wa leo linaeleza kuwa
wananchi watamchagua Rais wa Zanzibar, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi
na madiwani. Jumla ya wapiga kura visiwani Zanzibar ni 503,193. Pia
wananchi wa Jimbo la Kijitoupele katika orodha hiyo watamchagua mbunge
baada ya uchaguzi wa Oktoba kutofanyika kutokana na kuchelewa kuwasili
kwa vifaa vya kupigia kura katika maeneo mbalimbali ya jimbo hilo.
Taarifa
iliyotolewa jana na Jecha ilisema vituo vyote vya kupigia vitafunguliwa
saa 1.00 asubuhi na kufungwa saa 10.00 jioni. Alisema Tume yake
imekamilisha taratibu zote muhimu zitakazowezesha wapiga kura kupiga
kura bila ya usumbufu. “Hivi ninavyozungumza, vifaa vyote muhimu
vinavyohusika na kazi ya kupigisha kura tayari vimesambazwa katika vituo
vyote vya kupigia kura Unguja na Pemba,” alisema Jecha.
Alisema
uchaguzi wa leo umefuata sheria na aliwataka wananchi wote kuzingatia
ipasavyo maelekezo ambayo yametolewa na yatakayotolewa na maofisa wa
Tume, watakaokuwepo vituo vya kupigia kura. Alisema maelezo hayo
yanalenga kudumisha utulivu wakati wote wa kupiga kura, kuhesabu na
kujumlisha kura katika vituo. Alitoa mwito kwa wapiga kura, wagonjwa na
ambao hawawezi kupiga kura wenyewe, waruhusiwe kwa mujibu wa sheria
kwenda vituoni na watu wanaowaamini, ili kuwasaidia kupiga kura.
Alifafanua
kuwa mtu ataruhusiwa kumsaidia mtu mwingine kupiga kura baada ya mpiga
kura kumridhisha msimamizi wa kituo kuwa kweli hawezi kupiga kura na
anahitaji msaada wa mtu mwingine. Mwenyekiti huyo wa ZEC ambaye amekuwa
haonekani hadharani tangu atangaze kufuta matokeo ya uchaguzi wa Oktoba
mwaka jana, alitahadharisha kuwa ni kosa kubwa kwa mwananchi kutaka
kupiga kura kabla ya kituo kufunguliwa au baada ya kufungwa, au mtu
anayetaka kupiga kura wakati hana haki ya kufanya hivyo.
Aliwahakikishia
wananchi kuwa Tume inafanya kila linalowezekana ili kuuendesha uchaguzi
wa leo kwa salama na amani na pia itahakikisha kuwa uchaguzi huo
unakuwa huru na wa haki. Naye Ofisa Mdhamini wa ZEC, Pemba Ali Mohamed
Dadi alipozungumza na waandishi wa habari katika Ofisi ya Tume Chake
Chake Pemba, amesema maandalizi yamekamilika kwa kazi za usambazaji wa
vifaa.
Dadi
alifafanua kwamba vituo 463 vitatumika kwa ajili ya wapigakura ambapo
katika kituo cha Mkoani vipo vituo 117, Chake Chake vituo 122 wakati
katika kituo cha Micheweni 91 na Wete vipo vituo 133. “Maandalizi ya
uchaguzi wa marudio katika kituo cha Pemba yamekamilika na kwa upande wa
Tume ya Uchaguzi Pemba tumeweka vituo 463 ambavyo vitatumika kwa wapiga
kura kutekeleza demokrasia ya kuchaguwa viongozi wa vyama vya siasa,”
alisema.
Waangalizi
wa kimataifa Jecha alisema ukiondoa waangalizi wa ndani ambao tayari
wametuma maombi yao ZEC pia utaangaliwa na waangalizi wa kimataifa
kutoka Umoja wa Afrika (AU), waangalizi kutoka Jumuiya ya Afrika
Mashariki, Umoja wa Tume za Uchaguzi za Nchi za Kusini mwa Afrika
(ECF-SADC), Commoro na ubalozi wa Zambia ambao tayari wamewasili
visiwani hapa.
Kauli
ya CUF na CCM Chama cha Wananchi (CUF) kimetangaza uchaguzi wa marudio
unaofanyika leo ni haramu na hawawezi kushiriki wala kutambua matokeo ya
uchaguzi huo. Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Ahmed Mazrui alisema hata kama
aliyekuwa mgombea urais wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad atashinda
kamwe hawawezi kutambua matokeo hayo kwa sababu wananchi wa Zanzibar
tayari walishaamua kupitia sanduku la kura.
Mazrui
alisema msimamo wa chama chake ni kuendelea kudai haki yao na
kuendeleza msimamo wao wa kutokushiriki uchaguzi wa marejeo kwa kuwa
wanaamini kuwa uchaguzi uliopita ulikamilika.
Naibu
Katibu Mkuu wa CCM, Vuai Ali Vuai amenukuliwa na vyombo vya habari
akielezea kuwa chama hicho kitaenda kushiriki uchaguzi wa leo kikiwa na
matumaini ya kushinda kutokana na maandalizi waliyofanya. Vuai
alinukuliwa akisema pamoja na vyama vingine kujitoa kwenye uchaguzi huo,
lakini anaamini kuwa vyama vilivyobaki vitatoa upinzani mkubwa kwa
chama chake.
No comments:
Post a Comment