Mbeya City inamuwinda mshambuliaji wa Prisons, Mohamed Samatta katika kuimarisha kikosi chake kwa msimu ujao.
Samatta tayari imefanya mazungumzo ya kuongeza mkataba mpya na Prisons ingawa mwenyewe amesema mazungumzo hayo hayamzuii kupokea ofa nyingine.
Kocha wa Mbeya City, Mmalawi Kinnah Phiri alipendekeza usajili wa Samatta ambapo alisema kuwa mchezaji huyo atasaidia kuziba pengo la Kenny Ally aliyesajiliwa na Singida United kwa madai ya kwamba uwezo wao kisoka unafanana.
Samatta msimu uliopita ameifungia Prisons mabao matano katika Ligi Kuu Bara.
Samatta alisema mkataba wake na Prisons ulikuwa wa mwaka mmoja, amefanya mazungumzo na viongozi ambapo anaamini kwamba watafikia muafaka na anafurahia maisha ya hapo kwa kipindi chote alichoishi na Prisons.
"Kuhusu Mbeya City pengine wao wameniweka kwenye mipango yao ila bado hawajaniambia jambo lolote, nimemaliza mkataba na Prisons tumezungumza ila bado hatua ya mwisho hivyo sizuiliwi kupokea ofa kutoka timu nyingine kwani mimi ni mchezaji huru."