Rais Magufuli amewaonya baadhi ya wanasiasa na kuwataka kufunga midomo yao wakati serikali inafanya kazi yake, Rais Magufuli amesema hayo leo wakati anazindua upanuzi wa bandari ya Dar es Salaam.
Rais Magufuli amewataka wanasiasa kuzungumza mambo wanayoyajua lakini si kuongea ongea tu vitu ambavyo hawavifahamu na kusisitiza kuwa baadhi ya watu ambao serikali inawashikilia katika vyombo vya usalama wanahusika na mauaji ambayo yanatokea mkoani Pwani.
"Lakini niwaombe pia na wanasiasa ambao wameshindwa ku 'contol' midomo yao na muda mwingine wanazungumza hata vitu wasivyovijua, unakuta mwanasiasa anasema watu wamekaa sana rumande anashindwa kuelewa Marekani wale watu wabaya walikaa Guantanamo miaka na miaka, lakini kwetu wanaposhikwa watu ambao wanahusika na mambo ya ajabu katika nchi kuna watu wanaongea ongea. Pwani kuna watu wamekufa kule zaidi ya 35 askari zaidi ya 15 na wanaohusika na vifo hivyo ni pamoja na hao waliopo rumande lakini mtu anatoka anasema watu wamekaa mno, unaweza kuona huyo mtu naye anahusika kwa namna moja au nyingine, wasitufanye tukafika hapo sababu wataumia, wajifunze kufunga midomo yao wakati serikali inafanya kazi yake" alisisitiza Rais Magufuli.
Rais Magufuli anasema kumekuwa na mzaha kwa baadhi ya watu kutokana na kuhongwa pesa ndiyo maana wao kazi yao ni kupinga kila kitu.
"Mimi nimetuma ujumbe huu ili uwafikie Watanzania na waelewe, tuna mambo makubwa tunashughulikia katika nchi hii, lakini kumekuwa na mzaha mzaha tu, unakuta muda mwingine mnashughulikia rasilimali za watanzania zinavyoibiwa , lakini unakuta mtu mwingine anapinga hadharani kwa sababu amepewa vijisenti, ninawaomba watanzania wote bila kujali itikadi za vyama vyao tutangulize masilahi ya nchi mbele, hujasimama hata siku moja kulaani mauaji yanayotokea huko halafu unaibuka unataka sifa za kisiasa eti hawa watu waachiwe, na bahati mbaya watu wanaokufa ni wa chama kimoja tu, nataka polisi mfanye kazi yenu."alisema Rais Magufuli
Mbali na hilo Rais Magufuli amewataka polisi kuwakamata watu wote ambao wanaongea ongea juu ya mambo hayo ili walisaidie jeshi la polisi katika upelelezi, bila kuwaogopa kwa sura, wala mwendo wao.