Baada ya TCRA kufanikiwa kuwaondolea wananchi KERO ya kusikilizishwa matangazo kwa lazima pindi wanapopiga simu, kuna taarifa kuwa wameitaka pia Kampuni ya Simu ya tiGO kufuta tangazo lake la JAZA UJAZWE kwa sababu linaenda kinyume na maadili na utamaduni wa kitanzania. Kuna tetesi watu wengi wameripoti kukerwa na tangazo hilo la kuudhi, hivyo TCRA wameitaka kampuni hiyo kulifuta mara moja kutoka kwenye mabango na matangazo ya sauti (televisheni, redio, yutube, santuri, nk).
MAONI YANGU
Kama kweli TCRA wamefikia uamuzi huo mimi nawaunga mkono kwa 101%. Ni ukweli usiopingika kuwa lugha iliyotumika kuandaa tangazo lile inakosa staha na adabu. Hata ikitokea baba na familia yake wanatazama TV sebuleni, tangazo hilo linapoanza tu baba huzima TV mara moja au kubadilisha chaneli.
Nawapongeza TCRA kwa uthubutu huu wa kuwaondolea kero wananchi hivyo kwenda sambamba kabisa na sera ya serikali ya “Tanzania ya Viwanda”. Nchi haiwezi kufikia malengo ya kuanzishwa viwanda wakati wananchi wanakwazwa na vitu kama hivi. Aidha, wananchi wataenda kinyume na maagizo ya Rais ikiwa tangazo hili litaendelea kuruka hewani na kutazamwa na watu wengi.
Kumbuka kwamba Rais ameagiza wasichana wanaopata mimba wasiruhusiwe kuendelea na masomo katika mfumo rasmi wa elimu; na watu wanaosababisha mimba hizo imeagizwa wafungwe jela miaka 30! Kwa kuwa tangazo la tiGO linachochea mafataki kuwajaza wanafunzi wa kike chips kuku na kisha kuwajaza mimba (JAZA UJAZWE), kusitishwa kwa tangazo hili kutapunguza idadi ya wasichana wanaojazwa mimba na mafataki. Vilevile, katazo la tangazo hili kutapunguza idadi ya mafataki wanaofungwa jela kwa sababu ya kuwapa mimba wanafunzi, hivyo kupunguza msongamano wa wafungwa katika mahabusu na magereza zetu.
Viva TCRA