DAR ES SALAAM: Wengi wamekuwa wakijiuliza sababu ya watoto wa Mzee Salehe Kiba, Ali Salehe Kiba, Abdul Kiba na Zabibu Kiba kuongozana kwenye kuoa na kuolewa lakini hatimaye siri imevuja kuwa, mama yao ndiye aliyechagiza hilo ili kuwapa radhi zake.
Akizungumza na Ijumaa juzikati, mmoja wa wanafamilia ya Kiba aliyeomba hifadhi ya jina lake alisema kuwa, Ali Kiba na Abdu Kiba hawakuwa na mpango wa kuoa katika siku za hivi karibuni lakini mkwara wa mama yao ndiyo uliwasukuma kufanya hivyo.
“Kuna wakati mama yao alikuwa hana furaha kabisa na akiulizwa anasema, anaumia kuona wanaye umri unakwenda lakini hawaoi, wanaishia kuonekana na wasichana na kuzaa nao tu, alikuwa akiumia sana.
“Alitamani sana kuona wanaye wanaingia kwenye ndoa haraka na alikuwa akiwaeleza kila wakati kuhusu hilo. Sasa ili kumfurahisha mama yao ndipo wakaamua kuwa waoe tena kwa kufuatana, ndiyo maana unaona ndoa zao zimeongozana. “Na Zabibu naye siku si nyingi anaolewa, ilikuwa naye aolewe baada ya Abdu kisha wafanye sherehe ya harusi ya pamoja lakini kuna vitu vimekwamisha hilo,” alidai mtoa habari huyo aliyeomba hifadhi ya jina lake.
Katika kile kilichoonekana kuwa, sababu ya ndoa hizo kufuatana ni mkwara wa mzazi, Ijumaa liliwahi kufanya mahojiano na mama wa Kiba ambaye alifungukia hilo la kutamani kuona wanaye hao wanaingia kwenye maisha ya ndoa.
Alisema: “Nitahakikisha mwaka huu (mwaka jana mwishoni) hauishi wanangu watakuwa wameoa, hilo ndilo litanifanya niwe na amani moyoni mwangu.” Gazeti hili lilifanya jitihada za kuwapata Ali na Abdu kwa nyakati tofauti ili kujua kama kuoa kwao kuna msukumo mkubwa kutoka kwa mama yao lakini hawakuweza kupatikana mara moja.
Hata hivyo mwandishi wetu alimtafuta Zabibu kuzungumzia ndoa yake ambapo alipopatikana alisema kuwa, kuhusu yeye kuolewa hilo suala likiwepo Watanzania watajua tu ila kwa sasa ni Ali na Abdu.
TUJIKUMBUSHE
Ali Kiba alioa Aprili 19, mwaka huu nyumbani kwa bibi harusi, Mombasa nchini Kenya huku Abdul Kiba naye akiolea Bongo, Aprili 22. Zabibu Kiba yeye yuko kwenye uchumba na mchezaji wa Timu ya Baroka FC ya Sauzi Afrika, Abdi Banda na inadaiwa siku si nyingi nao wataoana.
Source:Gazeti la Ijumaa
No comments:
Post a Comment