Vitisho vya Afisa Habari wa vinara wa Ligi Kuu Tanzania Bara Simba SC, Haji Manara kuelekea kumalizika kwa mashindano ya ligi kuu vimegonga mwamba baada ya mkutano wake alioutangaza kufanya hii leo Aprili 30, 2018 kushindwa kufanyika bila ya kutoa sababu maalum ya jambo hilo.
Manara amebainisha hayo kupitia taarifa yake aliyoitoa leo asubuhi kwa vyombo vya habari nchini Tanzania na kusema anaomba radhi kwa usumbufu wowote utakaojitokeza kutokana na kughairisha mkutano huo ambao alipanga kuzungumzia mikakati yao ya kutafuta alama 4 ili waweze kutambulishwa rasmi kama mabingwa wa mashindano ya Ligi Kuu Tanzania Bara kwa mwaka 2017/ 2018 baada ya jana kikosi chake kumchapa Yanga bao 1-0.
"Idara ya habari ya klabu ya Simba inawaomba radhi kwa kuwatangazia kuwa leo Jumatatu hakutakuwa na 'Press' kama ilivyotangazwa kwenu kupitia ukurasa wa instagram wa Mkuu wa idara ya habari Ndg Haji S.Manara. Tunawaomba radhi kwa usumbufu wote utakaojitokeza kwa kuhairishwa kwa mkutano huu wa leo, hivyo tunawaomba ndugu waandishi wa habari tuwe wavumilivu hadi hapo tutakapowatangazia siku nyingine ya mkutano", amesema Manara.
Simba mpaka sasa bado wanaongoza kilele cha msimamo wa ligi kuu Tanzania Bara kwa jumla ya alama 62 wakiwa wameshacheza mechi 26, nafasi ya pili ikishikiliwa na Azam FC kwa alama 49 akiwa na michezo 26 huku Mabingwa watetezi Yanga wakishikilia nafasi ya tatu kwa pointi 48 na michezo 24.
No comments:
Post a Comment