• Seynation Updates

    Tuesday 5 April 2016

    FREEMASONS WAJA NA MBINU MPYA YA KUWANASA WANACHAMA WAPYA, WATANZANIA WAPO ZAIDI YA 650

    Imebainika kuwa, taasisi inaayodaiwa kuwa na imani yenye utata duniani ya Freemason inaanza kupungua nguvu kufuatia wafuasi wake kuachana nayo na kurejea kwenye imani zao za mwanzo, chanzo kikiwa kusemwa vibaya kwa taasisi hiyo. 


    Kwa mujibu wa memba mmoja wa Freemason jijini Dar es Salaam, idadi ya wafuasi wa taasisi hiyo inapungua siku hadi siku na sasa viongozi wake wanahaha kutoa elimu ya kuwafanya waliobaki waendelee kubaki. 


    “Unajua wakati inaanza Taasisi ya Freemason ilipata jina kubwa sana kwani watu wengi maarufu walijiunga, lakini sasa yale manenomaneno kwamba kuna ibada ya kishetani, wanaojiunga wanatoa makafara ndugu zao, mara kuna chakula cha damu, baadhi ya wanachama wakaanza kutoka kurejea kwenye imani zao za awali,” alisema memba huyo. 


    Alipoulizwa kwa nini wafuasi wamekuwa wakiondoka kwa maneno mabaya ya watu kama kweli hakuna ibada, mwanachama huyo alisema: 


    “Sifa mbaya, unajua wengine waliona kama wanachafuliwa lakini ukweli wanaujua wao kwamba hakuna ibada za kishetani. Ila tunapokutana wote tunakuwa na maneno ya pamoja kama kuashiria mshikamano wetu.” 


    KUNA WANACHAMA WANGAPI TANZANIA? 
    “Kwa Tanzania mpaka sasa kuna wanachama wasiopungua 650. Unajua kikubwa ni masharti ya kujiunga wengi yanawabana, ndiyo maana idadi ni ndogo kwa nchi kama hii yenye watu wasiopungua milioni arobaini.” 


    WANACHAMA HAO NI AKINA NANI? 
    “Wafuasi wetu wengi wanatoka katika sehemu mbalimbali, kuna walimu, wauguzi, madaktari, watu maarufu, wafanyabiashara wakubwa na wengine ni wanafunzi wa ngazi ya chuo. Lakini tofauti na watu wanavyosema kuwa, kuna viongozi wakubwa wa serikali, si kweli. Viongozi wakubwa wa serikali si wafuasi wetu ila wanaweza kutoa ushauri au kusaidia pale inapobidi.” 


    KUMBE JENGO LAO LILIKUWA LA BUNGE ZAMANI 
    Katika mazungumzo hayo, memba huyo alisema kuwa, jengo linalotumiwa kama Ofisi ya Freemason lililopo maeneo ya Posta jijini Dar es Salaam, lilikuwa la bunge wakati wa mkoloni na baadaye serikali ya Tanganyika huru, mwaka 1961. 


    ILI KUJIUNGA UNATAKIWA KUWA MILIONEA 
    Tofauti na watu wanavyodai kwamba, unaweza kujiunga na Freemason ukiwa maskini halafu ukawa tajiri, lakini mwananchama huyo alisema kuwa, anayetaka kuwa mfuasi ni lazima aweze kutoa mchango unaofikia shilingi milioni kuanzia kumi na kuendelea. 


     
    KAULI YA SIR ANDY CHANDE YATOA NGUVU 
    Maneno ya memba huyo yanashibishwa nguvu na aliyewahi kuwa kiongozi wa Freemason ukanda wa Afrika Mashariki, Jayantilal Keshavji Chande ‘Sir Andy Chande’. 
    Akizungumza wakati fulani jijini Dar es Salaam kwa kuanika hali ya Freemason nchini na duniani kwa ujumla, Sir Chandy alisema kuwa, Tanzania ina wafuasi zaidi ya 600 ambao wanatokana na kada mbalimbali wakiwemo watu maarufu, lakini alisema hakuna viongozi wakuu wa serikali. 


    WANACHAMA WA FREEMASONS HAWATAMBULIKI 
    Chande alisema kuwa, si kazi rahisi kumtambua mfuasi wa Freemason lakini wao wenyewe ndiyo wanaofahamiana na kukutana katika vikao mbalimbali ambavyo hufanyika mara moja baada ya siku thelathini. 


    JE, IDADI YA WANACHAMA INAPUNGUA? 
    Baada ya kuulizwa swali hili, Chande alisema kuwa, awali tangu kuanzisha kwake mpaka miaka ya karibuni, wafuasi wa Freemason walifikia 8,000,000 duniani kote lakini kwa sasa wamefikia 6,000,000 kutokana na watu kuielewa vibaya taasisi hiyo. 


    WAFUASI WANATAKIWA KUBAKI NA IMANI ZAO 
    Sir Andy Chande alikwenda mbele kwa kusema kuwa, ili uwe mwanachama wa Freemason ni lazima mtu huyo aendelee kuwa muumini wa Mungu katika imani yake ya Kikristo au Kiislam. 


    UMRI NI JE? 
    Alisema anayetaka kujiunga awe na umri unaozidi miaka 21 na walio chini ya umri huo hawaruhusiwi kwa sababu ya uwezo wa kutunza mambo lakini pia akasema ili ujiunge Freemason ni lazima familia ya anayetaka kujiunga ua ndugu zake wajue ili kuepuka matatizo utakapotakiwa kutoa michango. 


    Gazeti la UWAZI NA SHEHE MKUU WA MKOA WA DAR ES SALAAM 
    Akizungumza na gazeti la UWAZI la hapa Tanzania juzi kuhusu imani hiyo kuwataka wafuasi wake wabaki kwenye imani zao, Shehe Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhadi Mussa Salum alisema: 
    “Muumini wa Kiislam, akiwa Freemason ajue si Muislam tena. Wale wana ibada mbaya, haitokani na Mungu tunayemwamini sisi. Wewe Kama ni Muislam halafu ni Freemason jiondoe kwenye Uislam.” 


    HUYU HAPA ZACHARY KAKOBE 
    Akizungumza na gazeti hilo la Uwazi Jumamosi iliyopita kuhusu imani ya Freemason, Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel &Bible Fellowship, Zachary Kakobe alisema: 
    “Ni unafiki mkubwa kumtumia Mungu aliyeumba mbingu na nchi halafu wakati huohuo ukawa kwenye imani ya Freemason. Chagua moja, Mungu hataki mtu vuguvugu. Kuwa moto au kuwa baridi ijulikane moja. Na watu wajue kwamba, ibada yoyote nje ya Mungu wa kweli ni ushetani.” 


    KAMANDA SIRO ANAVYOSEMA 
    Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Siro yeye alisema: 
    “Freemason ni taasisi ipo kisheria. Ila mimi nataka kushughulika na hao watu mnaowaandika kwamba wanajipatia pesa kwa kuuza fomu feki za Freemason kwa njia ya utapeli. Siku moja nitavaa kiraia halafu nitakwenda pale ofisini kwao nje nikawakamate.” 


    NAIBU WAZIRI ANENA Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamadi Yusuf Masauni alipoulizwa juu ya madai kuwa Freemason wanadaiwa kuwa katika imani za kishetani alisema hayo ni madai na hawezi kuyazungumzia kwa sababu hana uhakika na hicho kinachodaiwa.

    No comments:

    Post a Comment

    VIDEO MPYA

    UMBEA MTUPUU

    MAPENZI