• Seynation Updates

    Tuesday 27 December 2016

    TUNAPOKWENDA, NGUMI ZA TANZANIA ZITABAKIA KUWA ZA FACEBOOK




    Na Saleh Ally
    USIKU wa kuamkia jana kulikuwa na mjadala mkubwa katika tasnia ya ngumi kuhusiana na pambano la jana la ngumi za kulipwa kati ya Francis Cheka dhidi ya Dulla Mbabe.
    Mjadala ulianza baada ya Cheka kutupia maneno kwenye akaunti yake akisema kwamba asingecheza mechi yake hiyo ya jana kwa kuwa alikuwa hajalipwa fedha yake na promota Siraju Kaike.


    Muda mchache Kaike naye akatupia na kusema Cheka asipopanda ulingoni hiyo jana angemfikisha mahakamani kwa kuwa tayari alishampatia nusu ya fedha alizotakiwa kuchukua.


    Kaike alionyesha picha mbili, moja Cheka akisaini mkataba na nyingine akihesabu fedha alizolipwa naye ambaye Kaike anaonekana akiwa pembeni kushuhudia mazoezi yote hayo yakifanyika.


    Baada ya hapo wadau wakawa wanajadili kwa kiasi kikubwa kuhusiana na suala hilo, kila upande ukisema lake. Wapo waliomuunga mkono Cheka na wengine walimshangaa na kumuunga mkono Kaike.


    Hilo limeendelea hadi jana kutwa nzima na ikionekana wazi hata kama pambano lingekuwepo, basi mambo yasingekuwa mazuri kwa Kaike ambaye inaelezwa alifanya kazi ya ziada kuhakikisha Cheka anapata dhamana wakati akikabiliwa na kesi iliyompeleka jela.


    Siku chache zilizopita, mjadala kwenye mchezo wa ngumi ulikuwa ni kuhusiana na suala ya Cheka kuamua kwenda kupigana ngumi nchini India na ndani ya siku nane alitakiwa kurejea na kupigana na Dulla.


    Kwa kiasi kikubwa ilionekana si jambo sahihi kwa bondia ambaye ni makini ambaye alitaka mambo yake kwenda kwa mpangilio kama ambavyo mchezo wa ngumi za kulipwa unavyoelekeza.


    Baada ya Cheka kupigwa India, gumzo la tuhuma kwamba huenda ile mechi ‘aliuza’ ndiyo maana akakubali kupigwa wakati akiwa na nguvu, likatawala pia. Yeye akakanusha na kutoa maelezo ambayo aliamini yalikuwa sahihi kulingana na hali halisi.


    Wengi wakawa wanasubiri siku ya pambano, kwamba mambo yataendaje au hali itakuwaje kwa kuwa kila upande unaonekana kuchanganyikiwa na kama kweli Cheka angeweza kufanya vizuri katika pambano hilo dhidi ya Dulla.


    Cheka amerejea amekwenda kupima uzito na hapo ndipo alipoanza kudai fedha zake. Anasema hajalipwa, promota anaonyesha akisaini na anahesabu fedha.


    Hapohapo, limeibuka gumzo jingine kwamba kuna ugomvi kati ya mapromota wawili, Kaike na Jay Msangi. Hali inayosababisha mvutano huo huku kila mmoja akitaka kutanua misuli kumuonyesha mwenzake yeye ndiye anajulikana sana, mwenye uwezo mkubwa kifedha au mtoto wa mjini zaidi.


    Kama utafuatilia vizuri, utagundua mchezo wa ngumi sasa unapoteza mwelekeo na bado kidogo tu wapenda ngumi wataanza kukaa kando na kuachana nao huku wakisubiri mapambano ya mabondia kama akina Klitschko na wengine ili wafurahie ngumi.


    Mchezo wa ngumi umetoka mikononi, sasa unakwenda midomoni na inaonekana imekuwa ni malumbano yanayofanana na hisia za muziki wa taarabu ambao asili yake ni kupashana kwa maneno na bora ni yule mwenye maneno mazuri yanayovutia lakini yanayopasha kwa njia yoyote ile.


    Mapromota hawapendani, mabondia wanafanyiana figisu, viongozi wa mashirikisho ndiyo usiseme, kila mmoja ana kundi au upande wake bila ya kujali au unafanya vizuri.
    Sasa mchezo wa ngumi, zaidi uko kwenye mitandao na hasa Facebook kuliko hata ulivyo ulingoni. Unakwenda huko kwa kuwa sasa umejaa malumbano zaidi badala ya vitendo na waliopo wanaonyesha kufurahishwa au kuvutiwa na malumbano hayo.


    Mnataka maendeleo ya mchezo wa ngumi kwa malumbano kila wakati. Tena mitandaoni huku mkionyesha wazi chuki miongoni mwenu ilivyochukua nafasi. Nyie ni watu hovyo kabisa ambao mmepewa nafasi na mmeshindwa kuitumia vizuri. Hovyo kabisa.

    No comments:

    Post a Comment

    VIDEO MPYA

    UMBEA MTUPUU

    MAPENZI