Hayo yamesemwa na Charles Boniface Mkwasa, Katibu wa Yanga katika mahojiano maalum na Bin Zubeiry Sports – Online asubuhi ya leo.
Mkwasa amesema kwamba hali ngumu ya kifedha inasababishwa na matatizo ya Mwenyekiti wao, Yussuf Manji kwa sasa dhidi ya Serikali.
Inadaiwa Akaunti zote za Manji na kampuni zake, ikiwemo kampuni mama, Quality Group Limited zimefungwa kiasi cha kusababisha hadi mfanyabiashara huyo mwenye asili ya Kiasia kuanza kuzifunga baadhi ya kampuni zake na kusimamisha baadhi ya miradi.
Charles Boniface Mkwasa amesema watahakikisha Yanga haikwami kwa namna yoyote
Manji pamoja na kuwa Mwenyekiti, lakini ndiye mfadhili mkuu wa Yanga tangu mwaka 2006 na Mkwasa amesema klabu imeathirika kwa kiasi kikubwa kutokana na matatizo hayo.
“Masuala mengine yote yanaendelea, hatuwezi kusema tuna kiasi gani au tunafanya vipi, lakini kama uongozi tunajaribu kufanya utaratibu wa timu iendelee na shughuli zake za kila siku,”amesema na kuongeza.
“Timu inakwenda, inakaa kambini na hatujaacha deni, kwa hiyo tunachokipata tunakitumia kwenye timu hicho hicho, vitu vikubwa ndivyo hatujaweza kufanikisha, lakini kwa masuala madogo kama ya kambi, na mambo mengine madogo madogo tunaweza kuyamudu,”.
Kuhusu mechi ya Raundi ya Kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Zanaco ya Zambia, Mkwasa amesema timu itashiriki mchezo huo bila wasiwasi.
“Tutacheza mechi ya nyumbani na tutasafiri kwa mechi ya ugenini hakuna shaka, Yanga ina viongozi wanaounda Kamati ya Utendaji, watakutana na kujadili na kujipanga,”alisema.
Aidha, Mkwasa amesema kwamba hakuna mchezaji anayeidai klabu, isipokuwa beki Vincent Bossou ambaye wakati mshahahara wake wa Januari unatoka alikuwa Gambia na timu yake ya taifa, Togo kwenye Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika.
“Tatizo mtu ambaye alikuwa ana cheki ya mshahara wa Januari wa Bossou (kutoka Quality Group) alitaka amkabidhi mchezaji mwenyewe cheki yake. Sasa Bossou amerejea anatakiwa kufuatilia mshahara wake Quality,”amesema Mkwasa.
Kuhusu taarifa za kwamba mchezaji huyo amegoma, Mkwasa amesema kwamba anasubiri taarifa ya benchi la Ufundi.
Pamoja na hayo, Mkwasa ameomba radhi kwa wanachama, wapenzi na mashabiki wa Yanga baada ya kufungwa mabao 2-1 na watani wa jadi, Simba SC juzi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
“Klabu inawaomba kuwa watulivu na pia inashukuru sana kwa utulivu waliouonyesha na kutii sheria zote kwenye mchezo wa Jumamosi, matokeo haya tuliyoyapata ni ya kimchezo kikubwa ni kupambana na michezo iliobakia mbele yetu na kuendelea kuwapa sapoti vijana wetu, kwani bado tuna mashindano mengi ma michezo mingi mbeleni,”amesema Mkwasa.
Mkwasa amesema anaamini kocha Mkuu, George Lwandamina ameona mapungufu kwenye mchezo huo na atayafanyia kazi kuelekea michezo ijayo na timu itafanya vizuri na kurejesha furaha ya wapenzi wake.
No comments:
Post a Comment