• Seynation Updates

    Friday, 5 May 2017

    TFF yabaki njia panda pointi za Simba.

    RAIS WA TFF, JAMAL MALINZI.

    WAKATI Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji ilitangaza kuipokonya Simba pointi tatu na mabao matatu walizopewa na Kamati ya Saa 72 ya Usimamizi wa Ligi Kuu, uongozi wa Kagera Sugar umesema bado hawajapata barua rasmi ya kurejeshewa pointi hizo.

    Akizungumza na gazeti hili, Meneja wa timu ya Kagera Sugar, Mohammed Hussein, alisema kuwa hadi jana klabu yake ilikuwa haijapokea barua yoyote inayowataarifu kurejeshwa kwa pointi hizo ambazo walipata uwanjani baada ya kuifunga Simba mabao 2-1 katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliofanyika Aprili 2 mwaka huu.

    Hussein alisema kuwa klabu hiyo haielewi pointi hizo kama zimerejea au wanazo Simba kwa sababu hawajapata taarifa rasmi ya uamuzi uliotolewa na Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji ambayo ilikutana baada ya wao kuomba kufanyika kwa merejeo ya uamuzi uliofanywa na Kamati ya Saa 72.

    "Mpaka leo (jana) hatujapata barua yoyote inayosema tumerejeshewa pointi, ila barua tuliyonayo mpaka muda huu ninaongea na wewe ni ile ya kupokonywa pointi tuliyopewa na Bodi ya Ligi," alisema Hussein.

    Aliongeza kuwa kitendo cha kutopata barua hiyo hadi leo kitaleta mkanganyiko wa idadi halisi ya pointi huku ligi hiyo inayotoa mwakilishi wa nchi katika mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa inakaribia ukingoni.

    Hata hivyo Simba kupitia Rais wake Evans Aveva juzi ilitangaza kuacha mchakato wa kwenda kupeleka mashtaka kwenye Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS) ikidai kupokonywa pointi tatu wakati Kagera Sugar ilimchezesha Mohammed Fakhi akiwa na kadi tatu za njano.

    "Tunachosubiri ni barua kutoka Bodi ya Ligi ili tujue tutakapoanzia," alisema Aveva naye akiweka wazi kuwa hawajapokea barua ya kupokonywa pointi tatu na mabao matatu kama ilivyoamuliwa na Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

    Aveva alisema wamefikia uamuzi wa kwenda CAS baada ya kujiridhisha kuwa Fakhi alikuwa na kadi tatu za njano na kanuni za ligi haziruhusu mchezaji mwenye kadi hizo kucheza mechi inayofuata.

    Endapo Simba itapata pointi hizo na kushinda mechi zake tatu zilizosalia ina nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu na vile vile kuchukua Kombe la FA kama itafanikiwa kumfunga Mbao FC kwenye mchezo wa fainali ya michuano hiyo utakaofanyika Mei 28 kwenye Uwanja wa Jamhuri Dodoma.

    VIDEO MPYA

    UMBEA MTUPUU

    MAPENZI