Yanga haijashunda wala kupata sare kwenye uwanja wa CCM Kirumba katika mechi mbili ilizocheza kwenye uwanja huo dhidi ya Mbao FC, imepoteza michezo yote miwili kwa timu hiyo ngeni kwenye soka la VPL.
Mara kwanza ilijikuta ikichapwa 1-0 na kutolewa nje ya michuano ya kombe la shirikisho Tanzania bara (Azam Sports Federation Cup) au FA Cup, kichapo hicho kilikuwa kwenye mchezo wa nusu fainali uliochezwa CCM Kirumba.
Wakati Yanga ikipambana kulipa kisasi siku ya mwisho ya kufunga ligi msimu uliopita May 2017, walichezea tena kibano cha bao 1-0 kwenye uwanja huohuo wa CCM Kirumba na kujikuta wakitangaza ubingwa huku wakiwa wamepoteza mchezo wao wa mwisho.
Mechi pekee ambayo Yanga walishinda dhidi ya Mbao ni ile ambayo walicheza uwanja wa Uhuru, Yanga ilishinda 3-0 kwa magoli ya Vicent Bossou, Amisi Tambwe huku bao la tatu golikipa wa Mbao akijifunga.
Nafasi kwenye ligi
Yanga ipo nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi ikiwa na alama 21 baada ya kucheza mechi 11, pointi tano nyuma ya Simba na Azam ambapo zinalingana kwa pointi kweny nafasi ya kwanza na ya pili.
Mbao ipo nafasi ya nane kwenye msimamo wa VPL, ina pointi 11 baada ya kucheza mechi 11. Mbao inalingana kwa pointi na timu tano chini yake (Kagera Sugar, Majimaji, Ndanda, MbeyanCity na Ruu Shooting) lakini yenyewe ipo juu kutokana na wastani wa magoli.
Pigo kwa Yanga faida kwa Mbao
Yanga itawakosa wachezaji sita kwenye mchezo wa leo dhidi ya Mbao (Yondani, Kamusoko, Ngoma, Ajib, Chirwa na Kakolanya) pamoja na kocha wao mkuu ambaye amerudi kwao Zambia kuhudhuria msiba wa mtoto wake.
Pigo hilo la Yanga kukosa nyota wake kadhaa huenda ikawa faida kwa Mbao kutumia mapungufu ya wachezaji kadhaa ambao ni wazoefu na wenye mchango mkubwa kwa Yanga.
Mbao yavimbia vigogo CCM Kirumba
Msimu huu bado Mbao haijapoteza mechi dhidi ya vigogo wa VPL (Simba, Azam) kwenye uwanja wa CCM Kirumba.
- Mbao 2-2 Simba
- Mbao 0-0 Azam
- Mbao ?? Yanga
No comments:
Post a Comment