Mfanyabiashara maarufu jijini Mbeya, Steven Samweli maarufu kwa jina la Maranatha, ametiwa nguvuni akituhumiwa kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Dhahiri Kidavashari, aliwaambia waandishi juzi kwamba, Maranatha alikamatwa juzi usiku akiwa katika moja ya maduka yake ya dawa baridi.
“Baada ya polisi kupata taarifa za mfanyabiashara huyo kuhusishwa na biashara ya dawa za kulevya, tuliweka mtego na hatimaye kufanikiwa kumtia nguvuni. Kwa sasa tunamshikilia kwa mahojiano na baada ya uchunguzi kukamilika, atafikishwa mahakamani,” alisema Kamanda Kidavashari.
Pamoja na hayo, kamanda huyo wa polisi alisema kukamatwa kwa mfanyabiashara huyo kunafikisha idadi ya watu nane waliokamatwa kwa tuhuma za kujihusisha na uingizaji, usambazaji na utumiaji wa dawa za kulevya mkoani Mbeya.
Aidha kamanda Kidavashari aliwataka wananchi waachane kabisa na biashara ya dawa hizo kwa sababu wakikutwa nazo, watakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya dola.
No comments:
Post a Comment