• Seynation Updates

    Wednesday, 19 April 2017

    ASKARI 17, VIONGOZI 18, WAMEUAWA MKURANGA KIBITI



    Idadi na watu, raia na askari polisi waliouawa kwa kupigwa risasi katika Wilaya za Rufiji, Kibiti na Mkuranga mkoani hapa imekuwa kubwa hivyo kutia wasiwasi kwamba, maisha katika eneo hilo ni ya roho mkononi, Uwazi limechimba na kuchimbua.

    Uwazi limebaini hayo kufuatia Aprili 13, mwaka huu, askari polisi wanane wilayani Kibiti kuuawa kwa kupigwa risasi kisha kuporwa bunduki 7 na watu ambao jeshi hilo linasema ni majambazi.

    Askari hao ni A/INCP Peter Kigugu, F.3451CPL Francis, F.6990PC Haruna,G.3447 PC Jackson, H.1872PC Zacharia, H.5503 PC Siwale, H.7629PC Maswi na H.7680PC Ayoub ambao wote wamezikwa Jumapili iliyopita.

    KWA NINI MKURANGA, KIBITI NA RUFIJI?

    Matukio ya askari kupigwa risasi wilayani humo si mageni lakini mbali na askari, pia viongozi wa vijiji wapatao 18 katika wilaya hizo nao wameuawa kwa kupigwa risasi. Inauma sana!

    WANANCHI WA KIBITI

    Wakizungumza na Uwazi baada ya mauaji ya askari hao, baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Mkengeni Kibiti, walisema kuwa, Mkoa wa Pwani umekuwa si salama kwa maisha ya watu na mali zao kwani mpaka sasa, hesabu za haraka zinaonesha kuwa, unaongoza kwa mauaji ya risasi huku viongozi na askari wakiwa wanashika namba kubwa.

    “Mimi kumbukumbu inaniambia, katika Mkoa wa Pwani na wilaya zake hizo, tayari askari kumi na saba (17) wameshauawa kwa kupigwa risasi na viongozi wa vijiji kama kumi na nane (18) nao pia wameuawa.

    “Hii idadi ni kubwa sana, siamini kama kuna mkoa umefikia, labda Dar es Salaam kwa sababu ya ukubwa wake wa makazi, lakini nje ya hapo sidhani,” alisema mkazi mmoja wa aliyejitambulisha kwa jina la Masaidi Khalidi. Anaongeza:

    “Jeshi la Polisi likitaka kumalizana na hii hali ni kuingiza ushirikiano na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), waingie msituni na kufanya kazi kama wako vitani, naamini wahalifu wote watakamatwa na itajulikana nguvu yao ilipo.”

    KUHUSU POLISI NI KWELI?

    Kufuatia madai hayo, Uwazi lilichimba kwenye kumbukumbu za nyuma na kukuta kweli idadi ya askari waliopoteza maisha Pwani inatisha, lakini pia idadi ya viongozi wa vijiji ambao pia wameuawa kwa kupigwa risasi pia inatisha.

    WALIANZA POLISI HAWA

    Juni 11, 2014, watu wenye silaha za jadi walivamia Kituo cha Polisi cha Kimanzichana, Wilaya ya Mkuranga mkoani hapa na kumuua kwa kumshambulia kwa mapanga askari Joseph Ngonyani kisha kupora bunduki tatu aina ya SMG na risasi 50.

    Mwaka 2015 nao ukaingia na balaa, matukio ya mauaji yaliendelea  kuukabili mkoa huu kufuatia askari wanne wa Kituo cha Polisi Ikwiriri kuvamiwa na kuuawa na watu ambao jeshi hilo lilisema ni majambazi. Askari hao ni Koplo Yahya Malima, Koplo Tito Mapunda,  Koplo Gaston Lupanga na Koplo Khatib Ame Pandu.

    KIZUIZI CHA POLISI VIKINDU

    Machi 30, 2015, saa 1:30 usiku wa kuelekea Sikukuu ya Pasaka, askari wawili waliuawa kwenye kizuizi cha barabarani katika Kijiji cha Kipara, maeneo ya Vikindu, Pwani. Waliouawa ni Sajenti Michael Aaron Tuheri na Koplo Francis Mkinga. Mauaji hayo yaliliacha jeshi la polisi nchini katika hali ya huzuni huku yakifananishwa na yale yaliyotokea katika vituo mbalimbali vya polisi nchini.

    IKWIRIRI TENA

    Januari 21, 2016, watu wasiojulikana walivamia Kituo cha Polisi cha Ikwiriri, Rufiji mkoani humu na kuwaua askari wawili, Koplo Edgar na WP Judith na kupora silaha zilizokuwepo kituoni hapo.

    KIJIJINI VIKINDU

    Agosti 26, 2016, askari wa ngazi ya juu katika kikosi cha kupambana na majambazi nchini, SSP Thomas Njiku aliuawa kwenye Kijiji cha Vikindu, Mkuranga akiwa katika oparesheni ya kuwasaka watu waliodaiwa kufanya uhalifu maeneo na Mbande, Temeke jijini Dar es Salaam.

    JARIBU MPAKANI

    Februari 22, 2017, taarifa kutoka Kibiti zilisema, mpelelezi wa wilaya hiyo (OC-CID), SP Peter Kubezya aliuawa kwa kupigwa risasi ya tumboni na watu hao wanaosadikiwa kuwa ni wahalifu. Tukio hilo lilijiri usiku wa saa 1, ambapo watu sita wenye bunduki  zinazosadikiwa kuwa ni aina ya Sub Machine Gun (SMG) walivamia Kituo cha Kutoza Ushuru wa Mazao ya Kilimo na Misitu Kijiji cha Jaribu Mpakani na kumuua kwa kumpiga risasi afande huyo na raia wengine wawili.

    KUHUSU VIONGOZI WA VIJIJI

    Kwa upande wa viongozi wa vijiji si rahisi kuamini lakini ndiyo ukweli ulivyo kwamba, idadi yao ilifikia kumi na nane (18) wakiwa wameuawa kwa nyakati tofauti. Usiku wa Machi 28, mwaka huu, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Tawi la Makondeko, Kijiji cha Ikwiriri Kaskazini, Emmanuel Lukanga aliuawa kwa kupigwa risasi.

    MUDA MCHACHE KABLA

    Akizungumza na Uwazi, kwenye mazishi ya kiongozi huyo, Katibu Kata wa Ikwiriri Kaskazini, Sauda Mningi alisema saa chache kabla ya Lukanga kufikwa na mauti walikuwa kwenye kikao cha kujadili suala la ulinzi na usalama wa eneo hilo.

    STAILI YAO YA KUUA

    Staili ya watoa roho hao ni kuua kwa risasi wakitumia bunduki aina ya SMG bila kuchukua pesa wala mali yoyote kutoka kwa marehemu huku wakiwa wamevaa kininja na wakitumia bodaboda hali inayotafsirika kuwa, ni mauaji ya visasi. “Huku jamani sisi wananchi, giza linapoingia wasiwasi tupu. Tunakuwa hatujui nani atauawa. Hawa watu wameanza zamani, tangu mwaka 2015,” alisema kiongozi mmoja huku akiomba hifadhi ya jina lake.

    VIONGOZI WALIPOKEA MESEJI

    Ilielezwa kuwa, viongozi mbalimbali wakitimia 18 wa vijiji vya wilaya hizo walianza kupokea meseji za vitisho kutoka kwa kundi moja la wahalifu wakidai roho zao ziko mikononi mwao, watawaua mmoja baada ya mwingine.

    MAUAJI YA KWANZA

    Mapema mwaka 2015, kundi hilo lilidaiwa kumuua kwa kumchinja karani wa Mahakama ya Mwanzo Mkuranga aliyetajwa kwa jina moja la Pazi.

    MACHI MOSI, 2016 Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyambunda, Said Mbwana aliuawa kwa kupigwa risasi na watu hao waliovamia nyumbani kwake. JULAI 17, 2016 Mwenyekiti wa Kijiji cha Kimanzichana, Ramadhani Mkagile naye aliuawa kwa kupigwa risasi na watu hao waliofika nyumbani kwake kwa njia ya bodaboda wakiwa wamevaa kininja.

    AGOSTI 12, 2016 Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Mkuruwili wilayani Mkuranga,  Salum Kiswamba ambaye pia alikuwa imamu wa msikiti, naye aliuawa nje ya nyumba yake kwa kupigwa risasi.

    OKTOBA 6, 2016 Katika Kijiji cha Kimanzichana, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi, Bakari Simkole akiwa ofisini, alipigwa risasi ya kifuani na kufariki dunia papohapo. OKTOBA 24, 2016 Kundi hilohilo lilimuua Mtendaji wa Kijiji cha Nyambunda, Ally Omar kwa kumpiga risasi akiwa nje ya nyumba yake.

    DESEMBA 6, 2016 Mohammed Ally Thabiti ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Kitongoji cha Nyambunda, Kijiji cha Nyang’hundu naye aliuawa kwa kupigwa risasi na watu waliovaa kininja.

    WAWILI WALIUAWA

    Nyuma ya mauaji ya viongozi hao wa kijiji hicho, waliuawa viongozi wengine wawili ambao Uwazi halikupata majina yao wala tarehe. Kijiji kikabaki hakina viongozi. JANUARI, 2017 Mauaji ya viongozi hao hayakuishia hapo, Januari mwaka huu, Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyambunda Wilaya ya Kibiti mkoani hapa, Said Mkandambuli naye aliuawa kwa kupigwa risasi na kundi hilo, nyumba yake imeota majani baada ya familia yake kukimbia.

    JANUARI 19, 2017

    Katibu Mtendaji wa Kijiji cha Nkwandala wilayani Kibiti (zamani kilikuwa katika Wilaya ya Mkuranga), Oswald Mrope naye aliuawa na wauaji hao ambao walimkuta akiwa amejipumzisha nje ya nyumba yake.

    FEBRUARI 9, 2017 Saa 6 usiku, kundi hilo linaloaminika kuwa ndilo linalotoa roho za viongozi, lilimuua Kamanda wa Mgambo Kata ya Bupu, Mussa Koti na kuichoma moto nyumba yake.

    SIKU HIYOHIYO

    Wauaji hao siku hiyohiyo walimuua kwa risasi, Kamanda Msaidizi wa Mgambo, Mohammed Cheleu na kuzichoma moto nyumba zake mbili, ya mke mdogo na mke mkubwa na kuacha ujumbe kupitia vipeperushi kuwa, roho zaidi zitaendelea kutolewa.

    FEBRUARI 21, 2017 Watu watatu walipoteza maisha (mmoja kati yao akiwa OC CID wa Kibiti) baada ya kuuawa na  kundi la watu wanaodhaniwa ni walewale wakiwa na silaha aina ya SMG/SAR. Mbali na OC-CID, wengine  ni Peter Kitundu aliyekuwa Mkaguzi wa Maliasili Kituo cha Jaribu  Mpakani na mgambo  aliyekuwa akifanya kazi za ulinzi kwenye kizuizi hicho, Athumani Ngambo.

    MACHI 12, 2017

    Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kazamoyo, Hemed Njiwa naye aliuawa kwa kupigwa risasi na watu hao akiwa nyumbani kwake.

    GAZETI LA UWAZI

    Gazeti la Uwazi, mara kadhaa tangu mwaka 2015 limekuwa likiandika habari za watu waliopo kwenye baadhi ya misitu kwenye wilaya hizo kwamba, ndiyo wanaopanga mauaji ya kutisha ya polisi kwa lengo la kuchukua silaha kwa matumizi wanayoyajua wao, ikiwemo kuwaua viongozi.

    KINACHOTOKEA

    Hata hivyo, licha ya mambo kuwa wazi, bado Uwazi limewahi kuitwa na uongozi serikalini na kuhojiwa juu ya habari hizo, hasahasa habari iliyowahi kuandikwa Julai 17, jana kwenye gazeti ndugu na hili, Amani yenye kichwa cha habari;

    WANAOJIITA AL QAEDA WAUA IMAMU WA MSIKITI.

    Katika habari hiyo, Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Mkuruwili Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani, Salum Kiswamba ambaye pia alikuwa imamu wa msikiti wa eneo hilo, aliuawa nje ya nyumba yake kwa kupigwa risasi na watu waliovalia kininja waliokuwa kwenye bodaboda.

    Katika kusema ukweli huu, baadhi ya viongozi serikalini hutaka kuamini kuwa, magazeti ya Global Publishers yanazua hofu huku ukweli ukiwa unaonekana.

    UWAZI NA BARUA KWA MAGUFULI

    Pia, Uwazi liliwahi kumwandikia barua Rais Dk. John Pombe Magufuli ikimweleza namna wananchi wa mkoa huo, hasa Mkuranga, Kibiti na Rufiji wanavyoishi kwa wasiwasi wakimwomba msaada wake kwa imani kwamba, anaweza kutuma jeshi maalum na kuwaangamiza wahalifu hao.

    KAMANDA KOVA ALIWAHI KUSEMA HAYA

    Kabla ya kustaafu kwake, aliyekuwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, CP Suleiman Kova aliwahi kusema kuwa kuna mtu anaitwa Hery, alihusika  katika kufadhili matukio ya mauaji huko Amboni (Tanga), Mkuranga (Pwani) na Stakishari (Dar) na mengineyo lakini aliongeza jeshi la polisi kwa  kutumia kikosi cha intelijensia kiliweza kubaini nyendo zake na kuinasa picha yake.

    UWAZI LILISEMA HOFU YATANDA MKURANGA

    Gazeti hilihili liliwahi kuandika mwaka 2015 kuwa, hofu kubwa imetanda wilayani Mkuranga hasa katika Kijiji cha Mamndi Mkongo kufuatia Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam kwa  kushirikiana na wale wa Mkoa wa Pwani kunasa silaha  za kivita zikiwa zimefukiwa kwenye shimo msituni. Tukio hilo  la unasaji wa silaha lilifanikiwa Agosti 29,  2015 katika msitu  mmoja uliopo  katika kijiji hicho  kilichopo umbali wa kilomita 23  kutoka mjini Mkuranga.

    SILAHA ZILIZOKUTWA

    Uwazi lilizungumza na kamati ya ulinzi na usalama kijijini hapo na kusema silaha zilizokutwa ni bunduki za kivita aina ya AK-47 (moja), SRA  (mbili), RPG (mbili) Greana (moja) na risasi 388, tambi za milipuko mikali, kitabu cha muongozo wa kijeshi, kemikali za kutengenezea mabomu ya kutupa kwa mkono na kitabu chenye maelekezo ya namna ya kujibadili mwanaume kuwa mwanamke au mwanamke kuwa mwanaume.

    Baadhi ya wananchi waliozungumza na Uwazi, wamemuomba Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Ernest Mangu kufuatilia kwa kina matukio hayo kwani yanawatia hofu wananchi.

    KUTOKA KWA MHARIRI

    Ni vyema jeshi la polisi likaongeza nguvu ya ulinzi ili kuhakikisha watuhumiwa wanakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria. Tunalaani mauaji haya kwa nguvu kubwa tukiamini kwamba, waliouawa hawakuwa na hatia!

    Credit - Uwazi/Globalpublishers

    VIDEO MPYA

    UMBEA MTUPUU

    MAPENZI