Katika kuonesha kwamba hawataki utani katika kuifanya timu yao izidi kuwa kubwa, klabu ya Real Madrid inajipanga kumchukua Antoine Griezman na Eden Hazard.
Inaeleweka kwamba kocha wa Real Madrid Zinedine Zidane ni mshabiki mkubwa wa Eden Hazard na amekuwa akitamani kumsainisha, lakini sasa jina lake lipo katika orodha ya juu kabisa ya wale wanaotakiwa Madrid katika dirisha lijalo la usajili.
Real Madrid wanaelewa kwamba kumng’oa Eden Hazard Chelsea sio kazi ndogo, lakini kutokana na uchaguzi wa raisi unaokaribia katika timu hiyo, raisi wa sasa wa Real Madrid anaweza kumtumia Hazard kama sehemu ya kampeni zake za kubaki raisi wa Real Madrid.
Kila mwaka linapofika suala la uchaguzi, wagombea wengi hujaribu kutumia kiasi kikubwa cha pesa kununua wachezaji wakubwa ili kuwapa imani mashabiki wa timu hiyo juu ya uwezo wake na ndicho Perez anachotaka kukifanya kwa Hazard.
Katika kuonesha kwamba Perez hataki mzaha gazeti la L’equipe la nchini Hispania limetoa taarifa kwamba klabu ya Real Madrid pia imeingia kwenye mbio za kumsajili nyota wa Atletico Madrid Antoine Griezman ambaye pia United wanataka kumsajili.
Griezman ndiye alifunga goli la kusawazisha katika suluhu ya bao moja kwa moja katika mchezo wa Madrid Derby. Lakini kumnunua Hazard na Griezman ndani ya dirisha moja la usajili itakuwa ngumu kutokana na bei zao na Madrid wameamua kuanza na Hazard huku Griezman akiwekwa kiporo hadi mwakani.
Griezman mwenyewe alipoulizwa kuhusu kuhama Atletico Madrid alisema swali hilo limemchosha kwani kila siku linajirudia na jibu ni moja, “ni kila siku swali hilihili hadi nashindwa kuelewa niwajibu nini, jibu langu ni lile lile ninalosema kila siku nina furaha hapa(Atletico) na najiona nikiwa hapa hapa” alisema Grizman.
No comments:
Post a Comment