• Seynation Updates

    Friday, 30 June 2017

    TUNAZIBA MAPENGO YA AJIRA -MAJALIWA

    Mh.Kassim Majaliwa

    Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amefunguka na kutoa ahadi kuwa serikali itaziba mapengo ya ajira kwa nafasi zote zilizoachwa wazi katika sekta mbalimbali kutokana na baadhi ya wafanyakazi kuacha kazi baada ya kubainika walikuwa wakitumia vyeti feki.
    Waziri Mkuu amesema hayo leo bungeni wakati akijibu maswali ya wabunge katika kipindi cha maswali na majibu kwa Waziri Mkuu, ambapo Mbunge Mbulu Vijijini, Flatei Massay alitaka kujua ni lini Serikali itaanza kutoa ajira ili kuziba mapengo ya watumishi ambao waliacha kazi kutokana na sakata la vyeti feki. 
    "Ni kweli kwamba tumepitisha zoezi hili la vyeti feki kwa watumishi wetu na baada ya kuwa tumekamilisha uhakiki huu tulipata makundi matatu, kundi la kwanza ni wale wenye vyeti feki moja kwa moja, kundi la pili ni wale wenye vyeti vinavyotumika na zaidi ya mtu mmoja na kundi la tatu ni utata wa majina ambao umejitokeza kwenye vyeti hivyo ila wao wamekata rufaa. Sasa wote hawa wameacha mapengo kwa sasa ila Mhe. Rais Magufuli ametoa nafasi za ajira zaidi ya hamsini elfu ili kuziba mapengo haya ambayo yamejitokeza kwenye vyeti feki lakini pia kuongeza ajira kwa lengo la kuboresha utoaji huduma" alisema Waziri Mkuu 
    Mbali na hilo Waziri Mkuu anasema kuwa tayari vibali vya ajira vimeshaanza kutolewa na Wizara ya Utumishi na kudai kwa kuanza wameanza na idara ya elimu ambapo tayari wameajiri walimu wa Sayansi ambapo tayari wamekwenda kwenye vituo vya kazi na kusema wametoa nafasi nyingine kwenye sekta ya afya, lakini Waziri Mkuu aliendelea kusisitiza kuwa vibali hivyo vitaendelea kutolewa kadiri ya nafasi ambazo Rais Magufuli ameahidi kwa Watanzania, ili kuziba mapengo na kuboresha pale ambapo kuna upungufu mkubwa. 
    Mwanzoni mwa mwezi wa tano mwaka huu serikali iliwasimamisha kazi watumishi 9,932 wa kada mbalimbali baada ya kubainika kuwa na vyeti feki, huku wengine wakitumia majina yanayofanana jambo ambalo limepelekea kukosekana kwa baadhi ya watumishi katika sekta mbalimbali. 

    VIDEO MPYA

    UMBEA MTUPUU

    MAPENZI