SIMBA SC imeanza Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na moto mkali, baada ya kuichapa mabao 7-0 Ruvu Shooting jioni ya leo Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Mshambuliaji Mganda, Emmanuel Arnold Okwi ameonyesha msimu huu amedhamiria kurudi kivingine katika Ligi Kuu, baada ya kufunga mabao manne na kuseti moja katika ushindi huo mnono.
Mabao mengine ya Wekundu wa Msimbazi, walio chini ya kocha Mcameroon, Joseph Marius Omog anayesaidiwa na Mganda, Jackson Mayanja yamefungwa na Shiza Ramadhani Kichuya, Juma Luizio Ndanda na Erasto Edward Nyoni.
Okwi alifungua sherehe za mabao dakika ya 18 akimchambua kipa Bidii Hussein baada ya pasi ya Muzamil Yassin na bao la pili akafunga dakika ya 22 baada ya kuwachambua mabeki ndani ya boksi kufuatia pasi ya kiungo Mnyarwanda, Haruna Niyonzima.
Emmanuel Okwi (kulia) amefunga mabao manne na kuseti moja katika ushindi huo mnono na Shiza Kichuya (kushoto) amefunga moja
Okwi akakamilisha hat trick yake dakika ya 35 baada ya pasi nzuri ya Muzamil tena kabla ya kusaidia kupatikana kwa bao la nne.
Okwi aliwatoka wachezaji wa Ruvu Shoting hadi karibu na boksi na kumpasia beki Erasto Nyoni pembeni kushoto, aliyetia krosi iliyosindikizwa nyavuni na winga machachari, Shiza Kichuya kuipatia Simba bao la nne dakika ya 42.
Mshambuliaji wa zamani wa Zesco United ya Zambia, Juma Luizio Ndanda akaifungia Simba bao la tano dakika ya 44 akimalizia krosi ya Nyoni, kabla ya Okwi kufunga bao lake la nne leo na la sita katika mchezo dakika ya 52 kwa kichwa akimalizia krosi ya kiungo Saidi Hamisi Ndemla.
Beki aliye katika msimu wake wa kwanza Simba SC baada ya kusajiliwa kutoka Azam FC, Erasto Edward Nyoni akakamilisha shangwe za mabao za Wekundu wa Msimbazi kwa kufunga la saba dakika ya 81.
Katika mechi nyingine za Ligi Kuu leo; bao pekee la mshambuliaji Mghana, Yahya Mohammed limeipa Azam FC ushindi wa 1-0 dhidi ya wenyeji, Ndanda FC Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara.
Mwadui imeshinda 2-1 dhidi ya Singida United Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga, Mtibwa Sugar wameilaza 1-0 Stand United Uwanja wa Manungu, Turiani, Morogoro na Mbao FC wameshinda ugenini 1-0 dhidi ya wenyeji, Kagera Sugar Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
Tanzania Prisons nayo imeibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mji Njombe na Mbeya City imeilaza Maji Maji ya Songea 1-0 katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.
Ligi Kuu inatarajiwa kuendelea kesho kwa mchezo kati ya mabingwa watetezi, Yanga SC kuikaribisha Lipuli ya Iringa Uwanja wa Uhuru.
Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Aishi Manula, Ally Shomary, Erasto Nyoni, Method Mwanjali/Juuko Murshid dk65, Salim Mbonde, James Kotei, Shiza Kichuya, Muzamil Yassin/Said Ndemla dk46, Juma Luizio, Emmanuel Okwi na Haruna Niyonzima/Mohammed ‘Mo’ Ibrahim dk43.
Ruvu Shooting; Bidii Abdallah, Said Madega/Amani George dk50, Yussuf Ngunya, Shaibu Nayopa, Mangasini Mbonosi, Baraka Mtui, Chande Magoja, Shaaban Msala, Ishara Said, Jamal Mtegeta na Khamis Mcha ‘Vialli’/Said Dilunga dk46.
Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Aishi Manula, Ally Shomary, Erasto Nyoni, Method Mwanjali/Juuko Murshid dk65, Salim Mbonde, James Kotei, Shiza Kichuya, Muzamil Yassin/Said Ndemla dk46, Juma Luizio, Emmanuel Okwi na Haruna Niyonzima/Mohammed ‘Mo’ Ibrahim dk43.
Ruvu Shooting; Bidii Abdallah, Said Madega/Amani George dk50, Yussuf Ngunya, Shaibu Nayopa, Mangasini Mbonosi, Baraka Mtui, Chande Magoja, Shaaban Msala, Ishara Said, Jamal Mtegeta na Khamis Mcha ‘Vialli’/Said Dilunga dk46.
TAZAMA VIDEO YA MABAO.:-
Saturday, 26 August 2017
MICHEZO
Home
MICHEZO
VIDEO: MITAMBO YA SIMBA IMEWASHWA, YAANZA LIGI KUU NA MOTO WA UBINGWA, OKWI APIGA NNE RUVU YAFA 7-0.(Mabao yote 7 ya mnyama Simba Vs Ruvu Shooting)