• Seynation Updates

    Monday 1 January 2018

    “Ukisikia Kakobe amezungumza, tafakari kwanza kabla ya kumkabili,”



    Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF), Zachary Kakobe amejibu hoja zinazotolewa dhidi yake, baadhi zikitolewqa na Serikali akisema anapozungumza ni lazima kutafakari kabla ya kumkabili.

    Askofu Kakobe alizungumza jana wakati wa ibada katika kanisa la FGBF lililopo Mwenge jijini Dar es Salaam.

    “Ukisikia Kakobe amezungumza, tafakari kwanza kabla ya kumkabili,” alisema.

    Kauli hiyo aliitoa ikiwa ni siku moja baada ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutangaza kuanzakufuatilia ulipaji wake wa kodi.

    Uamuzi wa TRAulitangazwa juzi na Kamishna Mkuu, Charles Kichere mbele ya waandishi wa habari baada ya hivi karibuni Askofu Kakobe kusikika akisema ana fedha nyingi kuliko Serikali.

    TRA ilisema uamuzi huo unatokana na kiongozi huyo wa kiroho kutokuwemo katika kumbukumbu za ulipaji kodi za mamlaka hiyo. Mamlaka hiyo ilisema kama utajiri wake unatokana na sadaka pekee litakuwa jambo la kushtua.

    Jana, Askofu Kakobe alitumia ibada hiyo kuwajibu TRA na pia alizungumzia mambo mengine mawili; uraia wake na onyo la Serikali la kuwataka viongozi wa dini kutokuzungumzia masuala ya siasa.

    “Tangu nilipoitika wito huu miaka 30 iliyopita, sijawahi kufanya biashara yoyote zaidi ya hii na kanisa hili halina mradi wowote wa kiuchumi. Kakobe hana mradi wowote na kama yupo anayejua ajitokeze aseme nitampa zawadi,” alisema Askofu Kakobe.

    “Akaunti yetu iko Benki ya NBC na iko chini ya Bodi ya Wadhamini, bodi ambayo imesajiliwa Rita (Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini). Kwa hiyo, hao wanaotaka kujua zaidi waende Rita wakaulize wajumbe wa bodi hii ni akina nani na waende NBC kuona vyanzo vyetu vya mapato kama ni tofauti na sadaka.”

    Huku akishangiliwa na waumini, alisema tatizo kubwa lililojitokeza nchini ni watu kutafasiri wanavyojua na kujikuta wakipotoka. Alisema hilo ni tatizo watu kutopenda kusoma Biblia kwa undani na kwa upana zaidi.

    “Wamemsikia Kakobe anazungumza hapa, anazungumza mambo ya rohoni kuhusu haya ya utajiri. Unaweza kusikia maneno ukatafsiri kivyako kwa sababu haya tunayozungumza hapa ni mambo ya rohoni, wewe unayatafsiri kisiasa,” alisema Kakobe.

    “Wanasema wewe una hela kweli kuliko Tanzania sema... ninaweza kuvunja hekalu na kulisimamisha kwa siku tatu. Mtu anajiuliza hekalu gani hili? Hekalu hili ni mwili wake. Maana yake niueni, nisulubisheni, lakini nitakufa na siku ya tatu nitafufuka, hii ndio hekalu, unatafsiri kwa akili.”

    Kwa sauti ya juu na yenye msisitizo, Askofu Kakobe alisema: “Kimsingi, mimi si mtu tu tajiri kuliko Serikali, bali ni tajiri kuliko Serikali zote duniani. Kwa hiyo ukisikia Kakobe amezungumza, tafakari kwanza kabla ya kumkabili.”

    “Hela yote ya Serikali ya Tanzania au dunia nzima haiwezi kununua tiketi hata moja ya Mbinguni. Mimi ni tajiri kuliko Serikali ya Magufuli (Rais John Magufuli) au Serikali ya Trump (Rais wa Marekani Donald Trump),” alisema.

    Alisema nyumba anayoishi iliyopo Kijitonyama karibu na Kituo cha Polisi Mabatini jijini Dar es Salaam aliijenga miaka ya sabini na tangu wakati huo hajawahi kujenga kokote na gari lake ni la kawaida.

    Askofu Kakobe alisema maisha yake si ya kifahari kama wasemavyo watu.

    Uraia wake
    Kuhusu uraia, Askofu Kakobe alisema wazazi wake walikuwa wakiishi Kakonko mkoani Kigoma na baada ya kufariki walizikwa huko, huku uraia wake ukifuatiliwa na ilibainika ni raia halali.

    “Baba yangu alikuwa mwalimu kwa kipindi kirefu, amefanya kazi Tanga, Sumbawanga, Usukumani kwa Wanyamwezi, Tabora na Shinyanga. Miongoni mwa watu tuliocheza pamoja katika utoto wetu ni Christopher Chiza, huyu alikuwa waziri,” alisema Kakobe.

    “Ukitaja kwa jumla familia yetu, inajulikana miaka mingi. Walikwenda kuchunguza uraia wangu na kujiridhisha pasina shaka na kusema huyu ni Mtanzania. Kuna kipindi watu walikwenda mara tatu kijijini kwangu Kakonko kuchunguza uraia.”

    Waumini wakiwa kimya wakimsikiliza, Askofu Kakobe alisema, ‘’ Nimezaliwa Tanzania, wazazi wangu wamezaliwa Tanzania, mimi ni Mtanzania kwa hiyo sitoki hapa, tutabanana hapa hana.”

    “Baada ya kuona, yote hayo, mara waende huku, waende huko waulize wazazi wangu ambao wamefariki hivi karibuni na makaburi yapo kijijini na niliwaambia makaburi wayaweke barabarani ili anayechunguza uraia wangu aanzie pale,” alisema.

    Alisema, ‘’Kila jambo chini ya mbingu kuna kusudi, kuna kusudi la Mungu mimi kuzaliwa Tanzania, kwa hiyo wanaosema nimetoroka hawanisumbui kichwa.”

    Kuhusu taarifa za kutoroka nchini alisema: “Ninapokwenda na kurudi washirika wa hapa wanajua. Kwa mfano safari ya mwisho ilikuwa Agosti (mwaka jana) na tangu hapo sijasafiri. Niko hapa na haya mengine nayasikia nimetoroka, hayanisumbui, ukiitwa majina si yako unasumbukia nini?”

    No comments:

    Post a Comment

    VIDEO MPYA

    UMBEA MTUPUU

    MAPENZI