Peralta amewahi kuchezea klabu ya Rangers ya Scotland |
Mchezaji wa timu ya taifa Honduras Arnold Peralta amepigwa risasi akiwa likizoni mji wake wa kuzaliwa wa La Ceiba.
Aliuawa katika maegesho ya magari katika mji huo, ambao unapatikana katika pwani ya taifa hilo.
Kiungo huyo wa kati wa umri wa miaka 26, ambaye amekuwa akichezea klabu ya Olimpia, katika mji mkuu Tegucigalpa, alichezea klabu ya Rangers ya Scotland hadi Januari.
Visa vya watu kupigwa risasi Honduras huwa juu sana na taifa hilo lina mojawapo ya viwango vya juu zaidi vya mauaji duniani.
Mkurugenzi wa michezo wa shirikisho la soka la Honduras Osman Madrid, alisema mauaji hayo ni ya kusikitisha na kwamba taifa hilo linaomboleza.
Haijabainika nini kilichosababisha mauaji hayo lakini polisi wanasema hakikuwa kisa cha wizi kwani hakuna kitu chochote kilichoibiwa.
Aliwakilisha Honduras katika Michezo ya Olimpiki 2012 jijini London lakini hakuweza kucheza Kombe la Dunia Brazil mwaka 2014 kutokana na jeraha.
Alitarajiwa kuchezea timu ya taifa mechi ya kirafiki dhidi ya Cuba wiki ijayo.
No comments:
Post a Comment