Tathmini hiyo imekuja baada ya timu hiyo jana kushinda mabao 3-2 dhidi ya Congo, katika mchezo wa kwanza wa raundi ya tatu na ya mwisho kufuzu fainali hizo, huku akionesha hofu juu ya kiwango kilichooneshwa na timu hiyo ya Congo kuwa cha juu.
Mkwasa amesema kitendo cha Serengeti Boys kuruhusu mabao mawili nyumbani ndicho kinachoifanya njia yake ya kufuzu fainali hizo kuwa ngumu, inagawa katika mpira wa miguu, lolote linaweza kutokea.
“Katika mpira kila kitu kinawezekana, vijana wamejitahidi kucheza vizuri lakini tatizo wameruhusu mabao mawili nyumbani, kwahiyo siyo rahisi kufuzu, ingawa lolote linaweza kutokea, na magoli yanaweza kufungwa katika uwanja wowote ule, uwe wa nyumbani, uwe wa ugenini, kila kitu kinawezekana, na tunawea kufuzu”
Nao baadhi ya wachambuzi licha kukiri kuwa timu ya Congo inakiwango cha juu zaidi ya kile cha Tanzania, wametoa maoni yao wakisema Serengeti Boys ina kazi kubwa kutoruhusu bao katika mchezo wa marudiano, kwani endapo itafungwa bao 1-0 itakuwa imeaga mashindano hayo.
Waziri wa Habari, Sanaa, Michezo na Utamaduni Nape Nnauye ambaye alikuwa bega kwa bega na timu hiyo kuelekea mchezo huo, ameonesha kufurahishwa na matokeo ya ushindi nyumbani, na kuwataka vijana hao wakapambane nchini Congo kuhakikisha wanafuzu michuano hiyo.
Katika mchezo huo wa jana ambao mashabiki waliingia bure uwanjani, Serengeti Boys ilipata magoli yake kupitia kwa Yohana Mkomola aliyefunga magoli mawili kipindi cha kwanza huku goli la tatu likifungwa na Issa Makamba kipindi cha pili.
Congo walifunga bao lao la kwanza kipindi cha pili kwa mkwaju wa penati uliopigwa na Langa-Lesse Percy baada ya beki wa Serengeti kumuangusha mchezaji wa Congo ndani ya 18, huku bao la pili likipatikana katika dakika za nyongeza kwa kros iliyomaliziwa kimiani baada ya kumpita golikipa wa Serengeti Boys, ilitokea upande wa kushoto.
Serengeti Boys itarudiana na Congo, Oktoba 2, mwaka huu, mjini Brazzaville na inahitaji sare aina yoyote ili kufuzu fainali hizo.
No comments:
Post a Comment